Tatizo la kucheleweshwa kwa haki lapatiwa ufumbuzi.

0
139

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameridhishwa na ujenzi wa jengo la Mahakama ya Tanzania, Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, Dodoma.

Rais Samia ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho kitakachoondoa tatizo la kucheleweshwa kwa utoaji haki kwa kuweka ofisi zote zinazohusika sehemu moja.

Jengo hilo litawarahisishia wananchi na wote wenye uhitaji wa msaada wa masuala ya haki na sheria kuweza kufuatilia masuala yao ndani ya muda mfupi kwani ofisi husika zitapatikana eneo moja ikiwemo huduma za mahakama kuu, mahakama ya hakimu mkazi, mahakama ya mwanzo, Polisi, mawakili na waendesha mashtaka.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza mahakama kwa kuja na ubunifu wa jengo la aina hii na kusema kuwa ameona thamani ya pesa iliyotumika.

“Nimeliangalia wakati napata maelezo nikaambiwa bilioni tisa… nilivyoingia ndani nimeziona bilioni tisa zilipokaa. Kwenye jengo hili thamani ya pesa kwa jengo ipo sawa sawa,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewataka watoa huduma katika jengo hilo kutenda kazi zao kama inavyopaswa na si vinginevyo.

“Jengo hili lina milango mitano ya madhumuni mbalimbali. Naomba milango ile itumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa na si majaji na mahakimu kupenya kukimbia wananchi wanaowasubiri kupata huduma kwao,” Rais Samia amesisitiza.

Mbali na uwepo wa huduma hizi, jengo hilo limewekewa miundombinu rafiki kwa walemavu na vyumba rafiki kwa wamama wanaonyonyesha.