TARURA yashusha neema Rungwe

0
162

Wananchi wa kata ya Mpuguso wilayani Rungwe, Mkoani Mbeya wameipongeza Serikali kwa kwa kuwajali baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara za Masebe-Bugoba-Lutete (KM 7.2) na Barabara ya Masabe DSP-Mpuguso TTC-Bugoba Kibaoni (KM5.0), zilizojengwa kwa kiwango cha lami.

Pongezi hizo zimetolewa na wananchi hao wakati wa ziara ya Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoani Mbeya wakikagua Mradi wa barabara za “Agri-Connect”, wenye lengo la kuboresha miundombinu ya barabara maeneo yanayolimwa mazao ya biashara.

Akiongea na wajumbe wa bodi hiyo diwani wa Kata ya Mpuguso Japhet Kagugu ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara hizo za lami ambazo zimeleta ukombozi na manufaa makubwa kwa vijiji vyote vinavyopitiwa na barabara hizo katika kata za Mpuguso, Isonda na Ilima.

“Kiuchumi barabara hizi zimetuletea manufaa makubwa katika kusafirisha mazao yetu ya chai, kahawa, ngano, Ndizi, viazi na parachichi. Kabla ya barabara hizi mazao yalikuwa yanaharibika kutokana na ubovu wa barabara, lakini kwa sasa mazao yanafika sokoni kwa uhakika na imesaidia kukuza kipato cha mwananch mmoja mmoja na pia Serikali imeongeza mapato,” amesema Kagugu.

Bodi ya Ushauri ya TARURA inaendelea na ziara ya kikazi mkoani Mbeya kukagua miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na iliyo kamilika ili kuhakikisha adhma ya Serikali ya kuboresha barabara za Vijijini na Mijini inatimia.