TANZIA: Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa afariki dunia

0
557

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kwa masikitiko makubwa ametangaza kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 24 Julai, 2020.

Rais Magufuli amesema Mzee Mkapa amefariki dunia hospitalini Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na mpendwa wao Benjamin William Mkapa.

“Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia, amefariki dunia katika hospitali Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele za haki, taarifa zingine zitaendelea kutolewa lakini Mzee Mkapa hatuanaye tena,” amesema Rais Magufuli katika taarifa yake kwa Taifa.

Wakati huo huo Rais Magufuli ametangaza siku 7 za maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo Ijumaa tarehe 24 Julai, 2020 kufuatia kifo cha Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.

Katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Taarifa zingine kuhusiana na msiba huu mkubwa kwa Taifa zitatolewa baadaye.