Tanzania yatoa mwelekeo sakata la COVID19

0
238

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa anakusudia kuunda kamati ya Wataalamu ambayo itamshauri juu ya hatua za kuchukua dhidi ya ugonjwa wa COVID19.

Rais amebainisha hilo mara baada ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali Ikulu jijini Dar es salaam.

“Nakusudia kuunda kamati ya Wataalamu, waliangalie suala la COVID[19] kwa upana wake. Waangalie remedies [njia] ambazo wanasema zitatusaidia, kwa upana wake kitaalamu kabisa halafu watushauri Serikali,” amesema Rais.

Amesema suala hilo halifai kulinyamazia bila kuwepo kwa utafiti wa kitaalamu ili waeleze upeo wa namna suala hilo lilivyo na mambo yanayopendekezwa.

“Hatuwezi kujitenga kama kisiwa na hatuwezi tu kupokea kinacholetwa bila kufanya utafiti wa kwetu,” ameongeza Rais Samia Suluhu Hassan.

Ugonjwa wa COVID19 ulianza kuenea duniani mwishoni mwa mwaka 2019 ambapo visa milioni 132 vimeripotiwa duniani kote, na kati ya hivyo, watu milioni 74.7 wamepona huku milioni 2.86 wakifariki dunia.