Rais John Pombe Magufuli ametangaza maombolezo ya Kitaifa ya siku 3 kuanzia leo tarehe 13 Juni, 2020 kufuatia kifo cha Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kilichotokea tarehe 09 Juni, 2020 nchini Burundi.
Katika kipindi chote cha siku 3 za maombolezo ya Kitaifa (kuanzia Jumamosi tarehe 13 Juni, 2020 hadi Jumatatu tarehe 15 Juni, 2020) bendera zote zitapeperushwa nusu mlingoti.
Rais Magufuli ameeleza kuwa Tanzania inatoa heshima hiyo kwa kifo cha Pierre Nkurunziza kwa kutambua kuwa alikuwa Rais wa nchi jirani ambayo imekuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri, wa kirafiki, kihistoria na kidugu na Tanzania.
“Burundi ni mwanachama mwenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Rais Nkurunziza aliipenda Jumuiya hii, pia aliipenda Tanzania na alishirikiana nasi kila ilipohitajika, hivyo nimeona Watanzania tuungane na ndugu zetu wa Burundi katika kuomboleza na kumkumbuka Rais Nkurunziza ambaye aliiona Tanzania kama nyumbani kwake” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amerudia kutoa pole kwa Mjane wa Rais Nkurunziza (Mama Denise Bucumi Nkurunziza), Familia, Serikali na Wananchi wote wa Burundi kwa kuondokewa na mpendwa wao, na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.