Tanzania yasisitiza ushirikiano kukabiliana na malaria

0
168

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inaendelea kuongeza jitihada mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa wa Malaria pamoja na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika (NTDs).

Makamu wa Rais amesema hayo huko Kigali Rwanda wakati wa mkutano uliolenga kuunganisha nguvu za pamoja katika kukabiliana na ugonjwa wa Malaria pamoja na magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele.

Ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa wadau ili kufanya uwekezaji katika upatikanaji wa kinga, upimaji wa magonjwa, matibabu, ufuatiliaji wa magonjwa pamoja na kuunganisha uvumbuzi na tafiti ili kuharakisha kufikia malengo na ahadi za mwaka 2018 ambazo zililenga kuondoa malaria katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola ifikapo mwaka 2023.

Pia Dkt. Mpango amesema Tanzania kwa sasa inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano wa programu ya kudhibiti magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele (2021 – 2026) unaolenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti na kutokomeza magonjwa hayo.

Amesema tayari mafanikio mbalimbali yamepatika nchini Tanzania katika udhibiti wa ugonjwa wa malaria ikiwemo kufikia chini ya asilimia moja kuenea kwa ugonjwa huo Zanzibar pamoja na mikoa mitano ya Tanzania bara ambapo lengo katika maeneo hayo ni kuondoa kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2025.

Makamu wa Rais yupo nchini Rwanda kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa 26 wa wakuu wa serikali wa nchi wanachama za Jumuiya ya Madola.