Tanzania yasisitiza sera rafiki katika kilimo

0
495

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema ili kuharakisha mabadiliko katika mfumo wa chakula, mataifa ya Afrika yanapaswa kuweka sera rafiki katika sekta ya kilimo.

Amesema sera hizo zitarahisisha upatikanaji zaidi wa fedha kwa vijana na wanawake, na hivyo wataweza kuvutiwa kushiriki katika sekta hiyo ya kilimo.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia Jukwaa la Wakulima, kwenye mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika wa mwaka 2022 (AGRF 2022) unaofanyika Kigali, Rwanda.

Amesema inapaswa kuwekwa kipaumbele katika ufadhili wa tafiti na maendeleo pamoja na huduma za ugani, zitakazosaidia kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo na hivyo kuhakikisha usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, ni muhimu ufadhili huo ukalenga uendelezaji wa rasilimali watu, kuvumbua mazao mapya pamoja na kukuza teknolojia rafiki kulingana na mazingira husika.

Makamu wa Rais yupo nchini Rwanda kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika wa mwaka 2022 .