Tanzania yashiriki mkutano kujadili madhara ya UVIKO19 kwa vijana

0
253

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Jukwaa la Nne la Vijana Duniani lililoanza leo jijini Sharm-El-Sheikh, Misri.

Akishiriki mkutano huo kwa njia ya mtandao Waziri Mkuu ameyaomba mataifa makubwa duniani yashirikiane na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ili kuhakikisha uchumi wa nchi hizo unarejea katika hali yake ya kawaida kutokana na madhara ya UVIKO-19.

“Tangu kuingia kwa wimbi la kwanza la UVIKO-19, tumeshuhudia athari kubwa za kiuchumi na hasa kwa vijana. Vijana wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu lakini uwepo wa UVIKO-19 umeathiri maendeleo ya sekta ya utalii ambapo vijana wengi wameajiriwa,” amesema.

Ameongeza kuwa UVIKO-19 umeathiri uwekezaji katika viwanda na kwenye sekta ya miundombinu ambako makampuni mengi yalitoa ajira kwa vijana lakini hayakuweza kufanya kazi na hivyo kuleta athari kubwa.

Amesema Tanzania imeonesha inahitaji kuungwa mkono katika jitihada zinazochukuliwa kwenye ujenzi wa miundombinu ili Watanzania na hasa vijana waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa jumla wa kitaifa.

Mkutano huo wa siku nne ambao unashirikisha wajumbe zaidi ya 5,000 kutoka nchi mbalimbali duniani, unalenga kujadili madhara ya UVIKO-19 kwa vijana na namna gani nchi zimeweka mikakati ya kukabiliana nazo katika shughuli za kiuchumi, mabadiliko ya tabia nchi, hifadhi za jamii, haki za binadamu na uhifadhi wa mazingira.