Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ukanda wa Maziwa Makuu Balozi Xia Huang jijini Nairobi nchini Kenya.
Katika mazungumzo hayo Balozi Huang amewasilisha salamu za pole za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kwa Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha Dkt. John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania na pongezi kwa kupokea kijiti cha Urais akiwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania.
Balozi Huang amesema Umoja wa Mataifa una matumaini makubwa na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuiongoza Tanzania na kuendeleza ajenda za ukanda wa Maziwa Makuu ambazo ni kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuendeleza juhudi za kulinda amani na kuimarisha usalama.
Ameipongeza Tanzania kwa mchango na ushirikiano mkubwa inaoutoa kwa Umoja wa Mataifa katika juhudi za kulinda amani na kuimarisha usalama kwenye maeneo yote yenye mapigano na makundi yanayohasimiana, na ameahidi kuwa umoja huo utaendelea kushirikiana na Tanzania kulinda amani ili maendeleo ya jamii na uchumi yastawi.
Kwa upande wake, Rais Samia amepokea salamu hizo za pole na pongezi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na amemuhakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na umoja huo katika juhudi za kulinda amani na usalama katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Amesema hali ya ulinzi, usalama na demokrasia nchini ni nzuri, na ameuomba Umoja wa Mataifa kuendeleza jitihada zake za kulinda amani na usalama katika maeneo yote yenye matatizo.
Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuushawishi Umoja wa Ulaya (EU) kuondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Burundi.