Serikali ya Tanzania imepokea Faru weusi Tisa kutoka nchini Afrika Kusini, ambao watapelekwa katika hifadhi mbalimbali nchini.
Faru hao wamepokelewa hii leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, – Constantine Kanyasu pamoja na viongozi wengine mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro( KIA).
Akizungumza mara baada ya kupokea Faru hao, Naibu Waziri Kanyasu amesema kuwa, tukio hilo ni la kihistoria kwa vile ni mara ya kwanza kupokea idadi kubwa ya Faru kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, ameongeza kuwa idadi ya Faru ilikuwa Kumi, ambapo faru mmoja kati ya hao alikufa wakati akiwa njiani kuletwa nchini.
Naibu Waziri Kanyasu amesema kuwa, Faru hao watalindwa kwa gharama yoyote ile ili kuhakikisha hawapungui kama ilivyotokea katika miaka 1970 hadi 1980.
Ameagiza Faru hao wafungwe vifaa maalum, vitakavyokua vikionyesha mienendo yao popote watakapokuwa.