Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zimesaini mikataba mitano ya mkopo wa masharti nafuu ya dola milioni 495.59 za kimarekani, ambazo ni sawa na shilingi trilioni 1.14.
Fedha hizo zitawezesha utekelezwaji wa miradi mbalimbali ukiwemo ule wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma utakaogharimu dola milioni 271.63 za kimarekani, ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Horohoro – Lungalunga – Malindi yenye urefu wa kilomita 120.8 kwa gharama ya dola milioni 168.76 za kimarekani na dola 55.2 kwa ajili ya programu ya utawala bora na kuendeleza sekta binafsi.
Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Katibu Mkuu wa wizara ya Fedha na Mipango Doto James amesema kuwa serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika zimekuwa na mahusiano mazuri ambayo yamewezesha kutolewa kwa mkopo huo wenye masharti nafuu.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa, uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa kwa kuwa utakuwa na urefu wa kilomita 3.6 na upana wa mita sitini.
“Uwanja huu wa Msalato jijini Dodoma utakuwa mkubwa wa kuhudumia ndege kubwa aina ya Dreamliner 17, na kama ni aina ya Airbus ni ndege 380, magari ya kawaida 472, na mabasi ya abiria 72, na ukimalizika utahudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka”, amesema Mhandisi Mfugale.