Tanzania yaongoza kwa miradi ya ujenzi

0
897
Muonekano wa maendeleo ya ujenzi wa barabara za juu (Ubungo Interchange) katika makutano ya Barabara za Morogoro, Sam Nujoma, na Mandela. Ujenzi huu utakapokamilika utapunguza foleni za magari kwa kiasi kikubwa, na kurahisisha shughuli za usafiri na ushafirishaji.

Wakati serikali ikiendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo hasa katika sekta ya miundombinu, ripoti ya ujenzi ya The Africa Construction Trends Report (2019) iliyoandaliwa na Kampuni ya Deloitte kutoka nchini Uingereza inaonesha kuwa Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na miradi ya ujenzi yenye thamani kubwa zaidi.

Ripoti hiyo iliyotolewa mwezi Januari mwaka huu inaonyesha kuwa Tanzania na Kenya zote zilikuwa na jumla ya miradi 51 mwaka 2019, lakini miradi ya Tanzania pekee ina thamani ya dola bilioni 60.3 za Kimarekani ambazo ni shilingi trilioni 139, huku miradi ya Kenya ikiwa na thamani ya dola bilioni 36 za Kimarekani ambazo ni shilingi trilioni 83.2.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa ujumla miradi yote katika nchi za Afrika Mashariki iliongezeka kwa asilimia 30.9 kati ya mwaka 2018 na mwaka 2019, ambapo miradi inayoendelea kutekelezwa ni 182.

Nchi za Afrika Mashariki zinajumuisha asilimia 40.3 ya miradi yote barani Afrika ambayo thamani yake ni sawa na asilimia 29.5 ya miradi inayotekelezwa Afrika.

Kwa sasa serikali ya Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji utakaozalisha megawati 2115, upanuzi wa barabara mbalimbali nchini ikiwemo ile ya Morogoro kutoka Kimara mkoani Dar es salaam hadi Kibaha mkoani Pwani yenye urefu wa kilomita 19.2.

Miradi mingine ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo awamu ya kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na inatarajiwa kuanza kutumika baadae mwaka huu pindi majaribio yatakayokamilika, pamoja na upanuzi, ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege.