Rais John Magufuli ametangaza siku Tatu za maombolezo ya Kitaifa, kufuatia kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe,-Robert Mugabe kilichotokea nchini Singapore alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika siku hizo Tatu za maombolezo zinazoanzia hii leo, bendera zitapepea nusu mlingoti.
Mapema hii leo, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) alimtumia salamu za rambirambi Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, familia ya Mzee Mugabe, Wananchi wa Zimbabwe, Waafrika na wote walioguswa na msiba huo mkubwa.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema kuwa, Afrika imepoteza mmoja wa viongozi jasiri, shupavu, mwanamajumui wa Afrika na mtu aliyekataa ukoloni.
Rais Magufuli ameongeza kuwa, Mzee Mugabe aliipenda Tanzania, alijenga uhusiano na ushirikiano wa karibu, kidugu na kirafiki na Tanzania tangu enzi za uongozi wa Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwamba Afrika itamkumbuka kwa jinsi alivyoshirikiana na viongozi mbalimbali kupinga ukoloni na ukandamizaji wa haki za Waafrika.