Tanzania yaomba kusamehewa madeni na China

0
206

Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China,-Wang Yi ameondoka nchini na kuelekea Ushelisheli baada ya kukamilisha ziara yake ya siku mbili.

Kabla ya kuondoka nchini hii leo, Waziri Wang Yi alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Dkt John Magufuli wilayani Chato mkoani Geita.

Mara baada ya mazungumzo hayo Rais Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa kipande cha kuanzia Mwanza hadi Isaka kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya ujenzi ya China Civil Engineering Construction Company (CCECC).

Kipande hicho ni cha tano katika mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, ambacho kina urefu wa kilometa 341 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwaka 2024 kwa gharama ya shilingi Trilioni 3.0617 zinazotolewa na Serikali.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Waziri Wang Yi ameipongeza Tanzania kwa juhudi zake za kujenga barabara na miundombinu mingine kama China ilivyofanya, na kwamba hatua hiyo itaisaidia Tanzania kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kama China.

Ameziagiza kampuni za China zinazofanya kazi za ujenzi nchini Tanzania kufanya kazi hizo kwa ubora.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameishukuru China kwa ushirikiano wake na Tanzania katika masuala mbalimbali, yakiwemo ya kiuchumi na amemhakikishia Waziri Wang Yi kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano huo kwa maslahi ya pande zote mbili.

Ameipongeza kampuni ya CCECC iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa reli kati ya Mwanza na Isaka na ameelezea matumaini yake kuwa kampuni hiyo itafanya kazi nzuri.

Amemshukuru Rais Xi Jinping wa China ambaye kwa kumtuma Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje, -Wang Yi kuja Tanzania kuwasilisha ujumbe wake, na kwamba nae amemtumia Rais Xi Jinping ujumbe ukiwa na masuala muhimu matatu ya kuendeleza ushirikiano katika uchumi.

Masuala hayo ni kuomba ufadhili katika miradi miwili ya uzalishaji umeme katika Mto Ruhudji na Mto Lumakali, na pia kujenga kilometa 148 za barabara kuu Visiwani Zanzibar.

Pia ameomba kupatiwa msamaha wa madeni likiwemo lile la Dola milioni 15.7 za Kimarekani lililotokana na ujenzi wa reli ya TAZARA, deni la Dola milioni 137 za Kimarekani lililotokana na ujenzi wa nyumba za askari na deni la Dola za Kimarekani milioni 15 lililotokana na ujenzi wa kiwanda cha Urafiki – Dar es salaam.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa Tanzania na China ni ndugu na marafiki wakubwa, ndio maana Tanzania imezipatia zabuni kampuni za China katika ujenzi wa miradi mikubwa, ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kampuni za China zilizofanya kazi Tanzania zimelipwa zaidi ya shilingi Trilioni 21 zilizotokana na kodi za Watanzania.

Ametoa wito kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji wa China kuwekeza nchini, na pia China kununua mazao ya Tanzania yakiwemo chai, kahawa, pamba na korosho.

Rais Magufuli pia amewahakikishia Wafanyabiashara na Wawekezaji wa China kuwa kwa kuwekeza Tanzania watajihakikishia soko kubwa la Afrika Mashariki lenye watu Milioni 165 na soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lenye watu takribani Milioni 500.