Tanzania yalipia bilioni 85 ununuzi ndege mpya tatu

0
287

Tanzania imeendelea kuboresha shirika lake la ndege kwa kununua ndege mpya 11, ambapo ndege nane mpya zenye thamani ya shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na malipo ya awali ya kwa ajili ya ndege tatu zilizosalia tayari yamefanyika.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameyasema hayo akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21 nakubainisha kuwa serikali imefanya malipo ya awali yenye thamani ya shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege hizo.

Mpango ameeleza kuwa kati ya ndege hizo tatu mpya, ndege mbili ni aina ya Airbus A220-300 na moja ni aina ya De Havilland Dash 8-400.

Katika mkakati wake wa kuzidi kujiimarisha ATCL imefanikiwa kuongeza idadi ya vituo vya safari za ndani ya nchi kufikia 13 na nje kufikia sita ambavyo ni Hahaya (Comoro), Entebbe (Uganda), Bujumbura (Burundi), Mumbai (India), Lusaka (Zambia), na Harare (Zimbabwe).

Aidha, serikali imekamilisha ukarabati wa karakana ya matengenezo ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na kugharamia mafunzo ya marubani (110), wahandisi (127) na wahudumu (125).