Tanzania yaishukuru China kwa kuendeleza ushirikiano

0
205

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), – Guo Yezhou Ikulu jijini Dar es salaam.

Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemshukuru Yezhou kwa kutembelea hapa nchini kwa mara ya pili na pia ameishukuru China kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri na Tanzania ikiwemo mchango mkubwa wa Chama cha CPC ambacho kinajenga Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Chuo hicho ni kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uongozi kwa nchi Sita zenye vyama vya ukombozi vilivyoshirikiana na CPC ambazo ni Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Afrika Kusini kupitia ANC, Zimbabwe kupitia ZANU – PF, Msumbiji kupitia chama cha FRELIMO, Angola chama cha MPLA na Namibia kupitia SWAPO.

Rais Magufuli pia amemuomba Yezhou kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China na Mwenyekiti wa CPC, -Xi Jinping kwa kutoa Tuzo kwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Dkt Salim Ahmed Salim, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuiwezesha China kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Amemuhakikishia Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa China kuwa, Sera za Tanzania kuhusu China hazijabadilika na kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo katika jitihada mbalimbali za maendeleo.

Mazungumzo hayo yamehudhriwa na Katibu Mkuu wa CCM Bashiru Ally na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke.