Mkutano mkuu wa Nane wa Nchi Wanachama wanaotekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa, umeipongeza Tanzania kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa mkataba huo.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo unaofanyika jijini Abu Dhabi kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Dkt Mary Mwanjelwa amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka 2018/2019 Tanzania imefanya maboresho mbalimbali yakiwemo ya mfumo wa sheria kuhusu ushirikiano wa kimataifa katika uchunguzi wa vitendo vya rushwa.
Amewaeleza Washiriki wa mkutano huo kuwa, kupitia maboresho hayo Tanzania kwa sasa inaweza kubadilishana taarifa za kiuchunguzi za vitendo vya rushwa kwa njia ya kielektroniki na mataifa mbalimbali.
Mkutano huo mkuu wa Nane wa Nchi Wanachama wanaotekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa, unahudhuriwa na zaidi ya Washiriki Elfu Moja na Mia Tatu kutoka nchi Wanachama wanaotekeleza mkataba huo.
