Tanzania na Zimbabwe kushirikiana katika sekta ya Kilimo

0
228

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa Zimbabwe ambaye pia ni Kamanda wa Jeshi la anga la nchi hiyo Perrance Shiri.

Akizungumza mara baada ya mkutano huo, Waziri Hasunga amesema kuwa miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni kuongeza ushirikiano katika sekta ya Kilimo baina ya Zimbabwe na Tanzania.

Ameongeza kuwa, nchi zote mbili zina uzoefu katika sekta ya Kilimo, hivyo uzoefu huo unapaswa kuhuishwa katika nchi zote ili kuwa na tija ya Kilimo na kuimarisha usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa Waziri Hasunga, ujumbe wa Wataalamu wa Kilimo kutoka nchini Zimbabwe ukiongozwa na Waziri wao wa Kilimo umeiomba Tanzania kuwaongezea Tani zaidi za Mahindi ili waweze kurudi nazo nchini humo.

“Jana wameshuhudia treni ya kwanza ikiondoka kuelekea Zimbabwe ikiwa imebeba Tani 1, 200 za Mahindi na wanategemea Tani 17,000 za awali ambazo wamechukua ziwasili mapema iwezekanavyo”, amesema Waziri Hasunga.

Kwa upande wake Waziri huyo wa Kilimo wa Zimbabwe Kamanda Perrance Shiri amesema kuwa, lengo la ziara yake nchini Tanzania ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mauzo ya mahindi kutoka Tanzania kwenda Zimbabwe.

Amemuomba Waziri Hasunga kuwa na ushirikiano wa pamoja kwenye sekta ya Kilimo hususani katika zao la mpunga na mazao mengine.

Rais John Magufuli aliingia makubaliano na Rais Emmerson Mnangagwa  wa Zimbabwe kuwa, Tanzania itaiuzia nchi hiyo Tani Laki Saba za mahindi kufuatia nchi hiyo kukabiliwa na upungufu wa chakula.