Tanzania na Rwanda zakubaliana kukuza biashara

0
151

Tanzania na Rwanda zimekubaliana kukuza zaidi biashara kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili, kwani kiwango cha sasa cha biashara kati ya nchi hizo mbili hakiridhishi.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan amesema hatua za ukuzaji wa biashara zitahusisha pia uimarishaji wa miundombinu ya biashara.

“Tumeona haja ya kukuza biashara na kuweka miundombinu ya kukuza biashara kwa sababu kiwango cha biashara tulichonacho hakiendani na rasilimali tulizonazo kwa nchi mbili lakini na uhusiano mzuri uliopo,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema kuwa Tanzania ni mshirika muhimu wa Rwanda hasa katika biashara na mawasiliano na hivyo kukuwa kwa biashara ni kuimarika kwa maisha ya wananchi wote.

Aidha, amemshukuru Rais Samia kutokana na utayari wa Tanzania kuendelea kuimarisha uhusiano ambao umewezesha raia wa Rwanda kuendelea na kampuni za Rwanda kushindana vizuri katika soko la dunia.

Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania, mwaka 2021 Rwanda ilikuwa nchi ya tatu kupitisha idadi kubwa ya mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, ambapo kati ya mizigo hiyo tani milioni 6.4 iliyopelekwa nje ya nchi, tani milioni 1.3 zilikwenda Rwanda.