Tanzania na Namibia wajadili SACREEE

0
156

Naibu Waziri wa Nishati, -Subira Mgalu na Naibu Waziri wa Nishati wa Namibia, – Kornelia Shilunga pamoja na ujumbe wake, wamekutana na kujadili kuhusu Kituo cha Nishati Jadidifu na Matumizi Bora ya Nishati cha nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SACREEE).

Naibu Waziri Mgalu amekutana na ujumbe huo jijini Dodoma, ujumbe ambao uko nchini kwa lengo la kuisisitiza Tanzania kutia saini makubaliano yaliyofikiwa na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika( SADC), kuhusu kuanzishwa kwa kituo hicho.

Katika mazungumzo hayo, Naibu Waziri huyo wa Nishati ameueleza ujumbe huo kutoka nchini Namibia kuwa, bado Tanzania haijasaini Makubaliano hayo ya pamoja ya utekelezaji wa kituo hicho cha Nishati Jadidifu na Matumizi Bora ya Nishati cha nchi zilizo Kusini mwa Afrika na kwamba itafanya hivyo pindi uamuzi wa kuanzishwa kwake utakapoidhinishwa na Marais wa nchi za SADC.

Naibu Waziri Mgalu amesisitiza kuwa, baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria juu ya uanzishwaji wa SACREEE, Tanzania itakua tayari kusaini
makubaliano hayo ili kuwezesha kituo hicho ambacho Makao Makuu yake yako nchini Namibia kufanya kazi.