Tanzania na Diplomasia ya Sayansi

0
62

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu amebainisha kuwa, Tanzania inatekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Sayansi kwa kushirikiana na mataifa mbalimbali katika miradi ya Sayansi na Teknolojia.

Dkt. Nungu amebainisha hayo nchini Afrika Kusini katika mkutano wa kimataifa wa Sayansi (World Science Forum) unaoendelea mjini Cape Town, ambapo wadau wa sayansi wamesisitizwa kutekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Sayansi Ili sayansi iweze kutatua changamoto ndani ya jamii kwa usawa.

Amesema kwa sasa Tanzania kwa kushirikiana na nchi nyingine ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wamekuwa wakitekeleza kwa pamoja miradi ya Sayansi na utafiti katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Kilimo ambapo baadhi ya miradi ipo katika Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA).

Mkutano huo wa kimataifa wa Sayansi unatarajiwa kutoka na maazimio ya namna ya kuendeleza sayansi kwa manufaa ya wote.