Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Doto James amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu mkoani Kigoma yenye urefu wa Kilometa 260, ni mkakati wa serikali ambao unalenga kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
James ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba miwili ya mikopo ya ujenzi wa barabara hiyo, mikataba iliyosainiwa baina ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB).
Amesisitiza kuwa barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu ni kiunganishi muhimu katika maendeleo na uboreshaji wa biashara ndani na nje ya nchi, hivyo ni muhimu ujenzi wake ukaharakishwa.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu mkoani Kigoma utafanyika kwa pamoja na ujenzi wa barabara ya Rumonge – Gitaza ya nchini Burindi ambayo ina urefu wa Kilometa 45, lengo likiwa ni kuboresha mtandao wa barabara za Afrika Mashariki.
Mikopo hiyo miwili kwa ajili ya ujenzi wa barabara
ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu mkoani Kigoma ina thamani ya Shilingi Bilioni 589.26, fedha
zilizotolewa na Benki ya Maendeleo
ya Afrika.
