Tanzania kuwaachia raia wa Ethiopia wanaoshikiliwa nchini

0
192

Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amemhakikishia Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde kuwa yupo tayari kuwaachia wafungwa wapatao 1,789 wanaoshikiliwa kwa makosa ya uhamiaji haramu hapa nchini

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati wa makutano na waandishi wa habari mara baada ya kuwa na kikao cha ndani na Rais Zewde katika Ikulu Ndogo ya Chato mkoani Geita

“Tanzania tuna wafungwa wengi kutoa Ethiopia ambao walikamatwa hapa kwa uhamiaji bila taratibu, tumezungumza, na sisi tunawaachia huru na wakitumia ndege zao wakimbizi wote watarudi kwao ili wakajenge Taifa lao, sisi hatuna masharti yoyote na hata wakiwataka leo nitawaruhusu waachiwe huru,” amesema Rais Magufuli

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa Ethiopia ni nchi ya kwanza Afrika katika ufugaji wa ng’ombe na Tanzania ni ya pili lakini Ethiopia imepiga hatua katika utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na ngozi

“Ethiopia ni nchi ya kwanza kwa wingi wa mifugo Afrika, sisi (Tanzania) ni wapili. Wao wanafaidika sana na uzalishaji wa bidhaa za ngozi ambapo sisi hatujafaidika sana, hivyo tunaomba tukajifunze kwao” ameeleza Rais Magufuli

Kwa upande Rais wa Ethiopia ameshukuru kwa uamuzi wa Rais Magufuli kwa kutoa msamaha kwa wafungwa wanaoshikiliwa hapa nchini na kuahidi kufanya taratibu za kuwarejesha wafungwa hao

“Tunashukuru sana kwa moyo maamuzi ya Rais Magufuli kuwaruhusu bila masharti yoyote wafungwa ambao ni raia wa Ethiopia, na sisi tutafanya namna ya kuwarejesha nchini Ethiopia.”

Rais wa Ethiopia amekuwa na ziara ya kiserikali kwa siku moja hapa Nchi ambapo amekutana na mwenyeji wake Rais Dkt. John Magufuli na kuzungumza mambo mbalimbali ikiwemo mambo ya kiuchumi na diplomasia.