Maadhimisho ya Falsafa ya KAIZEN kwa mwaka 2021 yanatarajiwa kufanyika nchini Tanzania kwa siku tatu ambapo nchi zipatazo 20 zinatarajiwa kushiriki maadhimisho hayo na kubadilishana uzoefu katika kukuza sekta ya viwanda na biashara.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari na wasanii meneja wa KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Jane Lyatuu amesema kwa mwaka huu Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia Agosti 24 hadi 26 na yatafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania bara, Profesa Kitila Mkumbo na kufungwa na Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka visiwani Zanzibar.
Amesema, maadhimisho hayo yatafanyika kwa njia ya mtandao huku washiriki wengine wakishiriki kwa kukutana na kueleza kuwa hiyo ni fursa kubwa kwa Watanzania katika kuvuta wawekezaji, kutangaza bidhaa pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Lyatuu amesema kuwa, kupitia maadhimisho hayo Tanzania inapata nafasi ya kujifunza kutoka nchi mbalimbali mbinu bora za kutumia falsafa ya KAIZEN katika kukuza sekta ya viwanda na biashara.
Katika mkutano huo kutakuwa na majadilano maalum na Tanzania itapata wasaa wa kuwasilisha sera na uendelezaji wa falsafa ya KAIZEN nchini pamoja na washiriki kupata nafasi ya kutembelea viwanda na kujionea namna falsafa ya KAIZEN inavyotekelezwa.
KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana ya ‘badilika’ kwa ubora/uzuri na hutumika katika biashara. Huhusu shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi, mfumo, michakato na nyanja zote za kuendesha biashara.