Tanzania kupeleka miundombinu ya mawasiliano DRC

0
235

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Tanzania iko tayari kupeleka miundombinu ya mawasiliano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika.

Waziri Nape ameyasema hayo jijini Lubumbashi, DRC alipokuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la fursa za Kibiashara na Uwekezaji katika sekta ya TEHAMA kati ya Tanzania na DRC lililoanza leo.

“Serikali ya Tanzania iko tayari kuleta miundombinu ya mawasiliano ya Tanzania hususani Mkongo wa Taifa ili kuiunganisha DRC na nchi jirani, tunaamini katika umoja na ushirikiano wa nchi zetu kushirikiana ili kufikia malengo ya kiuchumi ya nchi zetu na wananchi wetu kwa ujumla,” amesema Waziri Nape

Akizungumza katika kongamano hilo, Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Said Mshana amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji wa TEHAMA wa DRC kuwa Tanzania ni nchi iliyojipanga kufanya biashara na DRC.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amewataka washiriki wa kongamano hilo kushiriki kwa ukamilifu kwenye majadiliano, ili kuona fursa zilizopo baini ya Tanzania na DRC.

Kongamano hilo ni la kwanza kufanyika baina ya Tanzania na DRC na limeandaliwa na wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na wizara ya Posta na Mawasiliano ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kongamano hilo la fursa za Kibiashara na Uwekezaji katika Sekta ya TEHAMA kati ya Tanzania na DRC linafanyika ikiwa ni miezi miwili tu tangu viongozi wa nchi hizo mbili wakutane wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan huko DRC.