Tanzania kinara Uhuru wa vyombo vya habari

0
247

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofuata misingi, sheria na kanuni za uendeshaji wa vyombo vya Habari, na kwamba mpaka sasa Serikali imevipa uhuru vyombo hivyo kutekeleza majukumu yao.
 
Akizungumza wakati akifungua mkutano wa Waandishi wa habari jijini Arusha katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, Waziri Bashungwa amesema Serikali inafanya kila jitihada ili kuhakikisha Watanzania wanapata habari za kweli.
 
Akijibu hoja ya Jukwaa la Wahariri Tanzania ambalo lilidai kuna anguko la tasnia ya habari nchini, Waziri Bashungwa amesema kutokana na Tanzania kuwa na uhuru wa vyombo vya habari imefanikiwa kusajili vyombo vingi vya habari kuliko nchi yoyote Afrika akitolea mfano magezeti 246, Redio 194, Televisheni 53, Redio za mtandaoni 23 na Televisheni za mtandaoni 440.
 
“Ndugu zangu Wanahabari, nyinyi nyote ni mashahidi kuwa uhuru wa vyombo vya habari hapa Tanzania ni mkubwa ukilinganisha na nchi zingine, tumesajili vyombo vingi vya habari, lakini uhuru huo uendane na wajibu, naomba sana tuhabarishe kwa kufuata misingi ya sheria, ni muhimu kufuata sheria zilizopo ili kuepukana na baadhi ya  changamoto,” Waziri Bashungwa.
 
Kuhusu hali ya uchumi wa Waandishi wa Habari,  Waziri Bashungwa amesema kuwa  sheria  namba 12 ya huduma za  habari ya mwaka 2016 iliweka wazi uanzishwaji wa bodi ya Ithibati na Baraza Huru  ili kuweza kutatua changamoto za wanahabari kama vile kutokuwa na mikataba, bima ya afya na mishashara isiyoridhisha.
 
“Sheria yetu ya Huduma za Habari imeainisha kuwepo kwa bodi ya ithibati na baraza huru la habari, napenda niwataarifu tu vyombo hivyo vitaanza hivi karibuni, lengo ni kuwafanya Waandishi kuwa na sauti moja katika kusimamia kazi zao wenyewe na kukumbushana kufuata sheria,” amesema Waziri Bashungwa.
 
Akiongelea suala la taswira ya nchi Kimataifa, Waziri Bashungwa  amewataka Waandishi wa habari kuwa wazalendo na nchi yao kwa kutoa habari sahihi zitakazoijengea heshima Tanzania, na kuvutia uwekezaji pamoja na kujenga diplomasia imara ya kiuchumi.