Tanzania haina ukandamizaji wa uhuru wa habari

0
1875

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania hakuna ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari wala taasisi zisizo za kiserikali.

Amesema kuwa jambo hilo linadhihirishwa na uwepo wa jumla ya vituo vya redio 152, ambavyo kati yake ni vituo vitatu tu ndivyo vinavyomilikiwa na serikali.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee.

“Tunapenda kuwahakikishia kuwa, Serikali ya Tanzania inaongozwa na katiba na sheria za nchi ambazo zinatoa uhuru wa kujieleza na kupata habari,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Amesema kuwa mwananchi yeyote atakayeenda kinyume na sheria, serikali itamuwajibisha kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, serikali imeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na ule wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Ameongeza kuwa pamoja na kusimamia haki hizo, serikali imeendelea kutekeleza wajibu wake katika kuiwezesha jamii kuishi salama kwa amani na utulivu kwa kuzingatia sheria za nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa zoezi la kuwarejesha wakimbizi wa Burundi nchini kwao lilikuwa ni la hiari na limetekelezwa baada ya hali ya amani kurejea nchini humo.

Amesema kuwa hakuna sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi ambao kwa hiari yao wameamua kurejea nchini kwao ili wakaendelee na shughuli za kulijenga Taifa lao.

“Nasisitiza kuwa zoezi hili ni la hiari, tangu mwezi Septemba mwaka jana Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi na UNHCR imekuwa ikiwarejesha wakimbizi hao kwao,”amesema Waziri Mkuu.

Amefafanua kuwa zoezi hilo limekuwa likifanyika kwa kuzingatia usalama na utu wa wakimbizi hao.

Wakimbizi 52,283 wa Burundi wamerejea nchini kwao kati 81,281 waliokwisha jiandikisha.

Waziri Mkuu Majaliwa amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada baadhi ya nchi kuishutumu serikali kwa namna ilivyoendesha zoezi hilo.

Pamoja na kutoa ufafanuzi huo, Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa na washirika wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1967 wa kuwahudumia wakimbizi ili kufanikisha zoezi hilo la kuwarejesha makwao kwa hiari na kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.

Maadhimisho hayo ya siku ya Umoja wa Mataifa ambao umetimiza miaka 73 tangu uanzishwe, yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), -Alvaro Rodrigues pamoja na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.