Tanzania haijafikia lengo la uchangiaji damu

0
134

Damu ya binadamu haiwezi kutengenezwa kiwandani, hivyo damu yote inayotumika katika vituo vya kutolea huduma za afya hutoka kwa watu wanaochangia kwa hiari ili kuokoa maisha ya wapendwa wao na watu wengine.

Leo Juni 14 ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Kuchangia Damu Duniani, mahitaji ya damu nchini yanakadiriwa kuwa chupa 550,000 kwa mwaka 2022/2023 lakini idadi ya chupa zilizokusanywa hazijafikia lengo kwani mwaka 2020/2021 zlikuwa chupa za damu 330,000.

Kuchangia damu ni tendo la hisani ili kuokoa maisha ya wale wanaohitaji, na chupa moja ya damu inaweza kuokoa maisha ya hadi watu watatu.

Matumizi ya damu nchini ni makubwa hasa kwa makundi yafuatayo; akina mama wajawazito wanaopoteza damu wakati wa kujifungua, watoto wenye umri chini ya miaka 5, wahanga wa ajali za barabarani na wagonjwa wa saratani.

Hivyo kila mwananchi mwenye afya njema anasisitizwa kuchangia damu ili kuhakikisha akiba ya damu inadumishwa na hivyo kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji hasa katika kuunga mkono ajenda ya kupunguza vifo vya wajawazito nchini Tanzania.