Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), – Selemani Jafo amesema kuwa, uchaguzi wa Serikali za Mitaa uko palepale na utafanyika Novemba 24 mwaka huu kama ilivyopangwa, licha ya vyama vingine kujitoa kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Waziri Jafo ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari, ambapo pia ametoa taarifa ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu.
Amesema kuwa, zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo za kugombea Uongozi katika Serikali za Mitaa limeenda vizuri na Wananchi waliochukua fomu ni 555,036 na waliorejesha ni 539,993 sawa na asilimia 97.29 ya wananchi wote waliochukua fomu, na ambao hawakurejesha ni asilimi 2.7.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo, baada ya zoezi hilo kukamilika ulifuatia uteuzi wa Wagombea ambao ulilenga kuteua wenye sifa, waliokidhi vigezo na kufuata taratibu zote za ujazaji wa fomu za kugombea na kubandikwa kwa orodha ya Wagombea waliopitishwa katika hatua hiyo.
Wagombea pia walipata fursa ya kuwasilisha pingamizi zao kwa mujibu wa Kanuni, na kisha kukata rufaa kwenye Kamati za Rufaa za wilaya zilizoundwa kwa ajili ya kuratibu rufaa za Wagombea
Waziri Jafo amefafanua kuwa mpaka sasa Rufaa zilizowasilishwa kutoka kwenye vyama mbalimbali vya siasa ni 13,500 na zinafanyiwa kazi na Kamati za Rufaa za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo zoezi hilo linakamilika hii leo.
Akizungumzia baadhi ya vyama kujitoa kwenye Uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa ilihali Wanachama wao walishateuliwa ama kuwasilisha rufaa zao kwenye Kamati, Waziri Jafo amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi jina la mgombea likishateuliwa linabaki kwenye karatasi za kupigia kura Novemba 24 hata kama chama chake kimejiengua kushiriki kwenye Uchaguzi huo.