TAMISEMI yakanusha wakurugenzi wa halmashauri kuitwa Dodoma

0
518

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imekanusha madai yaliyotolewa na mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kuwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wameitwa Dodoma na Rais Dkt. Magufuli ili wapewe maelekezo maalum kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema taarifa hiyo ni ya uongo na wananchi wanapaswa kuipuuza.

Aidha, amesema kuwa TAMISEMI imesikitishwa sana na taarifa hiyo ya uongo ambayo imetolewa na mtu anayeomba dhamana ya kuongoza nchi, ambayo pia inalenga kuwakatisha tamaa wasimamizi wa uchaguzi kwa nia ya kuvuruga uchaguzi na kuharibu amani ya nchi kwa makusudi.

“Wakurugenzi wote wa halmashauri wapo katika vituo vyao vya kazi wakiendelea kutimiza wajibu wao wa kusimamia shughuli za maendeleo na kusimamia maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa kuzingatia miongozo mbalimbali kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” ameandika Nyamhanga katika taarifa yake.

Wananchi wametakiwa kujiepusha na vitendo vyovyote vyenye nia ya kuhatarisha amani ya nchi katika kipindi hiki cha uchaguzi na wakati mwingine wowote.