TAMISEMI yaagizwa kusimamia ununuzi wa vifaa kwa fedha za UVIKO

0
215

Rais Samia Suluhu Hassani amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa kusimamia tenda za ununuzi wa vifaa tiba na kazi zingine kupitia fedha za UVIKO – 19.

Akizungumza na wananchi wa mkoa wa Tabora kwenye ufunguzi wa barabara ya Nyahua –Chaya Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuna zabuni za ununuzi wa vifaa vya afya bado zinasuasua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Amefafanua kuwa mwisho wa matumizi ya fedha za UVIKO – 19 ni mwezi Juni mwaka huu, hivyo fedha zote zinahitajika kutumiwa kwa wakati ili kukidhi vigezo vya kupata fedha zaidi.

Amemuagiza Waziri Bashungwa kuhakikisha zabuni hizo zinafanyiwa kazi kwa wakati ili kazi hizo zikamilike kwa wakati.

“Ucheleweshaji wa zabuni hizo utasababisha fedha nyingi kutotumika kwa wakati na kusababisha ukiukwaji wa malengo ya fedha hizo, suala hilo litapelekea fedha kurudishwa na kukosa fedha nyingine za maendeleo, nakuagiza Waziri wa TAMISEMI kalisimamie hili.” ameagiza Rais Samia

Kuhusu matumizi ya fedha kwenye halmashauri, Rais Samia ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatumia fedha zinazotolewa na serikali kwa kazi zilizokusudiwa za kutatua kero za wananchi

Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwenye ngazi ya halmashauri lengo likiwa ni kutatua kero za wananchi katika sekta ya afya, elimu, maji hivyo zisimamie na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali.