Tamasha la Twenzetu kwa Yesu kufanyika Jumamosi

0
166

Vijana wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye Tamasha la Twenzetu kwa Yesu lililoandaliwa na Upendo Media ili waweze kujifunza masuala mbalimbali, ikiwemo kupata maarifa ya kujitegemea kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt Emmanuel Luvanda wakati akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

Dkt Luvanda amesema tamasha hilo limeandaliwa kwa lengo la kuwakutanisha vijana, kwani wataweza kushirikishana fursa mbalimbali na kujenga urafiki miongoni mwao.

“Hili Tamasha sio tu kuimba, bali tunawakutanisha vijana ili kujenga wigo mpana wa kujifunza mambo mengi,” ameongeza Dkt Luvanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Upendo Media Neng’ida Johanes amesema Tamasha la Twenzetu kwa Yesu linakusudia kutoa elimu kwa vijana ili waweze kujitambua na pia linalenga kuwaandaa kuwa viongozi bora wa baadae.

“Upendo Media kwa kushirikiana na Wadau wengine tumeandaa tamasha hili sio tu kuburudika, bali na kutoa elimu ya kiroho na mwili ili Taifa letu lipate viongozi waadilifu, waaminifu na wenye weledi, maana hao ndio wanaweza kuja kuwa viongozi bora wa nchi yetu,” ameongeza Johanes.

Tamasha la Twenzetu kwa Yesu limekuwa likifanyika Kila mwana na kushirikisha dini na madhehebu mbalimbali na kwa mwaka huu litafanyika Jumamosi Desemba 18 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Kauli mbiu ya tamasha hilo kwa mwaka huu ni You Are Chosen (umechaguliwa).