TAKUKURU yalia na rushwa ya ngono

0
324

Wanawake nchini wametakiwa kuwajibika katika kutokomeza vitendo vya rushwa hususani ya ngono inayodaiwa kushamiri katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo taasisi za elimu ya juu pamoja na maeneo ya kazi.

Afisa Mchunguzi Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mwanza, Maua Ally ametoa wito huo wakati wa kongamano la kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika mapambano dhidi ya rushwa ya ngono, ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Rushwa ya ngono inaelezwa kuwa na athari kubwa katika maendeleo ya kitaaluma pamoja na ufanisi katika sehemu za kazi na hivyo kuhitaji jitihada za dhati za kuitokomeza.

TAKUKURU mkoa wa Mwanza katika kukabiliana na tatizo hilo imehimiza ushiriki wa jamii katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.

Elimu hiyo imetolewa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya na Tiba jijini Mwanza ambacho kimeanzisha dawati maalum la jinsia ili kukabiliana na changamoto zinazowakumba wanafunzi ikiwemo rushwa ya ngono.