Wataalam 73 wanaotoa huduma katika vyanzo vya mionzi kwa ajili ya uchunguzi na tiba kutoka hospitali mbalimbali nchini, wanashiriki katika mafunzo ya usalama wa mionzi yanayoendeshwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) jijini Arusha.
Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku tano, ni mwendelezo wa mafunzo yaliyofanyika mwaka 2019.
Akifungua mafunzo hayo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Mionzi kutoka Tume hiyo Dkt Justine Ngaile amewataka washiriki hao kuhakikisha wanapata uelewa wa kutosha katika mafunzo hayo utakaowasaidia katika kuhakikisha wanalinda afya za Watanzania.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea washiriki ufahamu juu ya matumizi salama ya mionzi na jinsi ya kujikinga na madhara ya mionzi na pia kutambua viwango vya mionzi ambavyo ni salama kwa Wafanyakazi katika maeneo ya kazi ili kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na mionzi.
“Mtajifunza kwa kina masuala ya usalama wa mionzi katika maeneo ya kazi, kwani usalama wa mionzi ni nyenzo muhimu katika kulinda wagonjwa, wafanyakazi na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi, hivyo basi naamini mtajengewa uwezo mkubwa na watalaamu wa TAEC,” amesema Dkt Ngaile.
Dkt Ngaile amewahakikishia Wataalam hao wanaotoa huduma katika vyanzo vya mionzi kwa ajili ya uchunguzi na tiba kuwa, TAEC itaendelea kutoa mafunzo ya namna hiyo ili kuhakikisha inawalinda Watanzania dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza wakati vyanzo vya mionzi vinapotumika katika maeneo mbalimbali.