TAEC yaendesha warsha ya namna ya kudhibiti Urani

0
203

Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), inaendesha warsha ya kuboresha shughuli za kisheria na uhakiki ili kuboresha uwezo uliopo katika kudhibiti madini ya Urani.

Warsha hiyo ya siku Tatu iliyoanza hii leo, inafanyika katika Makao Makuu ya TAEC yaliyopo Njiro mkoani Arusha na lengo lake ni kujadili tathmini ya ripoti ya Sheria ya udhibiti na mahitaji ya leseni ya uchimbaji wa madini ya Urani.

Taarifa iliyotolewa na TAEC kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa, wakati wa warsha hiyo muhtasari wa uwepo wa madini ya Urani nchini pamoja na utayari wa utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini hayo katika siku zijazo utajadiliwa.

Akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Profesa Lazaro Busagala amesema kuwa, majadiliano ya warsha hiyo yanalenga kuandaa Sheria mpya itakayoweza kutumika katika uchimbaji wa madini ya Urani pamoja na kumlinda Mwananchi wa kawaida na madhara ya madini hayo.

Washiriki 29 wanashiriki katika warsha hiyo, Ishirini kutoka TAEC na wengine Tisa wanatoka katika Taasisi nyingine ambazo zinahusika na masuala ya madini ya Urani ikiwa ni pamoja na Wizara ya Madini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Madini.