TAEC yaendesha mafunzo kuhusu usafirishaji wa mionzi

0
158

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), inaendesha mafunzo ya siku tano ya kitaifa kuhusu utunzaji na usafirishaji salama wa vyanzo vyenye viasili vya mionzi kwa Watendaji wa taasisi mbalimbali zinazojihusisha na usafirishaji wa mionzi nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea mkoani Dar es salaam, Mkuu wa TAEC Kanda ya Mashariki Dkt. Wilbroad Muhogora amesema kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawasaidia  watendaji hao kupata ujuzi kuhusu utunzaji na usafirishaji bora na salama wa vyanzo vya mionzi.

“Usafirishaji wa vyanzo hivi unaweza kusababisha madhara iwapo matakwa ya kiulinzi na kiusalama hayatazingatiwa wakati wa kuvitunza au kuvisafirisha, kwa  hiyo mafunzo haya yatawasaidia kupata uelewa zaidi na kutayarisha mipango ya kinga mionzi wakati wote.” amesema Dkt. Muhogora.

Vifaa vyenye mionzi vimekuwa vikitumika nchini katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi ikiwemo afya, kilimo na viwanda, ambapo mpaka sasa idadi ya vifaa vinavyotoa mionzi nchini vinakaribia 900 na kati ya hivyo vyanzo vya mionzi vyenye viasili vya mionzi ni 400.