Taasisi zinazodaiwa na TANESCO zatakiwa kulipa madeni yao

0
163

Naibu Waziri wa Nishati,- Subira Mgalu ameziagiza Taasisi za Serikali zinazodaiwa madeni ya umeme na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kulipa madeni hayo ili Shirika hilo liendelee kutoa huduma bora kwa Watanzania wote.

Naibu Waziri Mgalu ametoa agizo hilo mkoani Simiyu, wakati akizungumza na Wakazi wa kijiji cha Gasuma wilayani Bariadi alipokwenda kuwasha umeme kwenye kijiji hicho.

Amesema kuwa TANESCO imepewa jukumu la kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kusambaza umeme katika maeneo yote ambayo bado hayajafikiwa na umeme nchini ifikapo Juni 2021, hivyo ikiwa wateja wake hawatalipa madeni yao ndani ya muda stahiki, kazi hizo haitafanyika kazi kwa ufanisi.

“Meneja wa mkoa, endelea kuchukua hatua za kisheria, nimeona tayari umeshaanza kuchukua hatua hizo, lakini hazitoshi, deni linazidi kukua endelea kuwachukulia hatua wale wote ambao hawajalipa madeni yao”, amesisitiza Naibu Waziri Mgalu.

Pia amewaagiza, Wakuu wa Wilaya kulichukua suala hilo la madeni ya umeme kwenye Taasisi za Serikali kama moja ya ajenda zao katika vikao vyao vya kila siku, kwani madeni yao yanaweza kusababisha TANESCO kushindwa kujiendesha.

Kuhusu mahitaji ya umeme mkoani Simiyu, Naibu Waziri huyo wa Nishati amesema kuwa, mkoa huo unahitaji umeme wa kutosha ili kutimiza lengo lake la ujenzi wa viwanda, hivyo katika mwaka huu wa fedha Serikali imeamua kujenga kituo cha kupoza umeme, kazi ambayo imekwishaanza.