Taarifa ya Kinana, Makamba na Membe kukamilishwa ndani ya siku Saba

0
446

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) imetoa muda wa siku Saba kwa kamati ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya chama hicho kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama wake Watatu ambao ni Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Bernard Membe ambao walihojiwa na kamati hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CCM, taarifa ya kamati hiyo ndogo itakapokamilika itawasilishwa kwenye vikao husika vya chama hicho.

Kamati Kuu ya CCM iliyokutana leo jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa imepokea taarifa ya awali kuhusu azimio la kuwaita na kuwahoji wanachama hao watatu.

CCM ilifikia azimio la kuwahoji wanachama hao waandamizi mwezi Disemba mwaka 2019 katika kikao chake jijini Mwanza kufuatia kukiuka kanuni za kinidhamu zinazoongoza chama hicho.

Membe ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje alihojiwa tarehe 6 mwezi huu jijini Dodoma, wakati Makatibu Wakuu wastaafu, Kinana na Makamba walifika mbele ya kamati hiyo tarehe 10 mwezi huu.