Taarifa ya awali ajali ya ndege yapokelewa

0
202

Kikao cha Baraza la Mawaziri kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan leo kimekutana jijini Dodoma ambapo kimepokea taarifa ya awali juu ya ajali ya Precision Air na hatua zilizochukuliwa mara baada ya ajali hiyo ya Novemba 6, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, Baraza la Mawaziri limewaelekeza wataalamu wa ndani kushirikiana na wataalamu waliotoka nje ya nchi kufanya uchunguzi wa ajali ili kujua chanzo cha ajali na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na ajali na majanga.

Taarifa imeeleza kuwa hilo ni kwa mujibu wa taratibu na sheria za kimataifa zinazoshughulikia ajali za ndege ambapo Tanzania imesaini makubaliano ya kutekeleza taratibu na sheria hizo.

Aidha, limeagiza vitengo vyote vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe.

Kwa mujibu wa taratibu za kukabiliana na ajali za ndege;

. Timu ya uchunguzi wa ajali na matukio ya ndege inapaswa kutoa taarifa ya awali (Accident Bulletin) ndani ya siku 14.

• Inafuatiwa na ripoti ya awali (Preliminary Report) itakayotolewa ndani ya siku 30

• Na hatimaye ripoti kamili (Final Report) itakayotolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea.

Baraza la Mawaziri limewashukuru wote waliohusika katika uokoaji baada ya ajali hiyo kutokea na limewaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi ukifanyika na utakapokamilika watajulishwa matokeo ya uchunguzi huo.

Katika ajali hiyo, watu 24 waliokolewa na 19 walifariki dunia baada ya ndege kuanguka Ziwa Victori wakati ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba.