Sumaye arejea CCM

0
404

Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye ametangaza kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni takribani miaka mitano tangu alipoondoka.

Sumaye ametangaza uamuzi huo leo Februari 10, 2020 katika kikao cha Baraza la Wadhamini, Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es salaam, na kupokelewa na Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ally.

Agosti 22 mwaka 2015 Sumaye alijitoa CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikiwa ni moja ya vyama vilivyokuwa vikiunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Baada ya kukitumikia chama hicho kwa zaidi ya miaka minne, Disemba 4 mwaka 2019 alitangaza kujitoa CHADEMA kwa kile alichosema kwamba alidhani ndani ya chama hicho kungekuwa na demokrasia lakini haikuwa hivyo.

Licha ya kujitoa CHADEMA alisema hajiungi na chama chochote cha siasa na kwamba angebaki huru na kuendelea kutoa ushauri kwa chama chochote ambacho kingemhitaji wakati wowote.

Miezi miwili baada ya kutoa kauli hiyo amejiunga CCM, akiwa ni kiongozi wa pili wa ngazi ya juu kurudi CCM baada ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowasa kurudi CCM mwezi Machi mwaka 2019 akitokea CHADEMA, chama alichojiunga nacho mwezi Julai mwaka 2015.