Stars yakwea pipa kuelekea Cameroon

0
203

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega amemkabidhi nahodha wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) John Bocco fedha za posho za ndani za wachezaji pamoja na bonasi ya mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Fedha hizo ni sehemu ya mchango wa Serikali kusaidia maandalizi Stars kuelekea mashindano ya CHAN 2021 nchini Cameroon.

Katika hafla ya kuiaga timu hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia leo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri Ulega pia amewakabidhi viongozi pamoja na wachezaji wa timu hiyo bendera ya Taifa.

“Serikali imechangia zaidi ya shilingi milioni 60 kama bonasi na posho za ndani za wachezaji na benchi la ufundi, bado tunapambana kupata fedha ili kusaidia katika maeneo mengine, TFF hakikisheni mnasimamia nidhamu ya matumizi ya fedha hizi pamoja na nidhamu kwa vijana ili timu yetu iweze kutuwakilisha vyema,” amesisitiza Naibu Waziri Ulega.

Taifa Stars imeondoa nchini leo alfajiri kuelekea nchini Cameroon kushiriki michuano ya CHAN 2021.