Stars, Mwakinyo watinga Ikulu

0
324

Rais John Magufuli ameahidi kuwapatia wachezaji wote wa Timu ya Taifa ya Soka (Taifa Stars) pamoja na Bondia Hassan Mwakinyo viwanja vya kujenga nyumba katika mahali pazuri patakapopatikana jijini Dodoma.

Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo Ikulu Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kuwapongeza wachezaji hao wa Stars,  baada ya kufuzu kucheza fainali za michuano ya Afrika kwa mwaka 2019 na kwa  Bondia Mwakinyo ni baada ya kumpiga bondia Sergio Gonzalez wa Argentina kwa TKO.

Akizungumza na wachezaji hao, Rais Magufuli amewataka kuongeza jitihada ili waweze kufanya vizuri katika michuano hiyo ya AFCON itakayofanyika mwezi June mwaka huu nchini Misri na hatimaye waweze kufika fainali.

Amewataka katika michezo yao yote watambue kuwa Watanzania ni wapenda michezo na wanatamani timu zao mbalimbali zifanye vizuri na kufika mbali.

Rais Magufuli amewapongeza watanzania wote kwa kuwa wazalendo kwa kuishangilia Taifa Stars na  kuwaomba kuonyesha uzalendo na mshikamano ya aina hiyo kwa timu zote ambazo zinakua zikishiriki mashindano ya Kimataifa.

Amevihakikishia vyama vyote vya michezo nchini kuwa serikali itaendelea kushirikiana navyo ili kuhakikisha michezo inafanya vizuri.

Kuhusu michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 inayofanyika mwezi Aprili mwaka huu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi Bilioni Moja kwa lengo la kuisaidia timu ya vijana ya Tanzania ili iweze kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Katika mchezo wake wa jana uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaa, Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania iliifunga Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) magoli matatu Bila na kupata tiketi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa Barani Afrika.

Hii ni Mara ya pili kwa Tanzania kufuzu fainali hizo, ikiwa imefanya hivyo pia mwaka 1980