Standard Chattered kutoa fedha zaidi ujenzi SGR

0
339

Benki ya Standard Chattered imeihakikishia Tanzania kuwa iko tayari kutoa fedha zaidi kwenye miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, ukiwemo wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege.

Ahadi hiyo imetolewa na uongozi wa benki hiyo ukiongozwa na Mwenyekiti wake Jose Vinals, ulipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango. Dkt. Mwigulu Nchemba kando ya mikutano ya majira ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa nayofanyika jijini Washington nchini Marekani.

Akizungumza mara baada ya mkutano huo Dkt. Nchemba amesema kuwa Benki hiyo ya Standard Chattered ilitoa mkopo unaotumika kujenga SGR kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida, na kwamba hivi sasa Serikali iko kwenye mazungumzo na benki hiyo ili itoe mkopo mwingine kwa ajili ya vipande vingine vya reli hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wacZanzibar, Saada Mkuya Salum amesema kuwa katika kuimarisha shughuli za utalii na kukuza uchumi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepanga kuboresha miundombinu ya uwanja wa ndege wa Pemba na kwamba mazungumzo yanayoendelea kati ya Serikali na Benki hiyo yatawezesha kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Standard Chattered nchini Tanzania, Sanjay Rughani amesema benki hiyo iko tayari kutoa fedha zaidi kwa ajili ya miradi iliyowasilishwa na Serikali kwenye Benki hiyo.

Amesema kuwa pamoja na ahadi ya kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, benki hiyo pia iko tayari kuwashawishi wawekezaji wengine kutoka maeneo mbalimbali duniani kuwekeza mitaji na teknolojia nchini Tanzania.

Februari 13 mwaka 2020, benki ya Standard Chattered iiliipatia Tanzania mkopo wa dola bilioni 1.5 za Kimarekani kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha kuanzia Morogoro hadi Makutupora, mkoani Singida.