Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema wameamua kufanya mkutano wa 53 wa Jukwaa la Mabunge ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC PF) mkoani Arusha kutokana na uwepo wa vivutio vingi vya Utalii.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan kufungua mkutano huo Dkt. Tulia amesema, mbali na vivutio vya utalii vilivyozunguka mkoa wa Arusha lakini pia hali ya hewa ya mkoa huo ni rafiki kwa wajumbe wengi wa mkutano huo.
Amesema Tanzania imekuwa katika harakati za kutangaza utalii wake na hivyo kusanyiko hilo litapata fursa ya kwenda kwenye vivutio vya utalii vilivyopo Kilimanjaro, Arusha na Manyara ili kuutangaza zaidi utalii wa Tanzania.
Mkutano huo wa siku saba unafanyika kwa mara ya nne hapa nchini ambapo kwa mwaka huu mada kadhaa zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na mada itakayoangazia njia za kisasa katika kilimo kama njia ya kuwa na uhakika wa chakula na ukosefu wa ajira kwa vijana.