Spika amuomba radhi Rais na Wananchi

0
146

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemuomba radhi Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kutokana na mijadala iliyojitokeza hivi karibuni katika mitandao mbalimbali ya kijamii inayoonesha kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaopinga jitihada zinazofanywa na Rais katika kuliletea Taifa maendeleo.

Spika Ndugai ameomba radhi jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari na kuongeza kuwa kazi inayofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kubwa na inapaswa kuungwa mkono na kila mtu.

Amesema anaunga mkono jitihada zote za Serikali ikiwa ni pamoja na kukopa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, na wanaomuona yuko kinyume basi wamemuelewa vibaya.

Spika Ndugai ameyasema hayo kufuatia kauli yake aliyoitoa tarehe 26 mwezi Desemba mwaka 2021 kuzua mijadala katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini, huku yeye akishutumiwa na baadhi ya watu kuwa anaenda kinyume na mipango ya Serikali.

Amesisitiza kuwa kauli yake kuwa nchi inaweza kupigwa mnada kutokana na kukopa ilikuwa utani wa Kigogo ili kuwataka Watanzania walipe tozo zitakazosaidia kujenga shule pamoja na zahanati.

Kuhusu fedha za UVIKO – 19 Spika Ndugai amesema Bunge limekuwa sehemu ya kukubaliana na hoja hiyo na kwamba hivi karibuni Wabunge wataeleza kazi kubwa iliyofanywa na fedha hizo katika majimbo yao.