Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema tayari imekamilisha kuandaa mihtasari kwa ajili ya somo jipya la Historia ya Tanzania litakaloanza kufundishwa Julai 2021, kama alivyoagiza Rais Dkt John Magufuli kufundishwa kwa somo hilo kwa madarasa yote.
”Tumekamilisha mihtasari yote na sasa vitabu vinaandaliwa kwa ajili ya kufundishia wanafunzi na tunatarajia hadi kufikia mwezi Machi vitabu vyote vitakuwa tayari,” amesema Waziri wa Elimu, Prof Ndalichako jijini Dodoma.
Amesema maandalizi ya vitabu vitakavyotumika katika kufundisha vinaandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo wabobevu katika historia ya nchi ya Tanzania.
“Maandalizi haya ya vitabu na historia tunashirikiana na Wadau mbalimbali katika kuandaa vitabu hivi hatufanyi peke yetu tumeshirikisha wizara mbalimbali na taasisi ili kufanya kwa uhakika zaidi ili somo hili jipya hapa nchini lifundishwe kwa ufasaha mkubwa,” amesema.
Amesema nchi ya Tanzania ina historia kubwa sana ambayo ikifundishwa kwa vijana wetu itasaidia kuwa wazalendo na kulinda rasilimali za taifa sambamba na kujua nchi ilipambana vipi katika kupata uhuru wake.
Amebainisha kuwa somo hilo litafundishwa kwa lugha ya Kiswahili kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita ili somo hilo liweze kueleweka vizuri kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Taknolojia, Dkt Leonard Akwilapo amesema kidato cha tatu, nne, na sita watasoma tu bila kufanya mitihani ila kwa kidato cha kwanza na kidato cha pili ndio watakaofanya mitihani.