Soko la Hollywood kufunguka kwa wasanii wa Tanzania

0
157

Wasanii nchini hasa wa muziki na filamu wameahidiwa kufunguliwa milango zaidi katika soko na kiwanda kikubwa cha burudani duniani cha Hollywood nchini Marekani, ili kupata mafanikio katika kazi zao.

Ahadi hiyo imetolewa nchini Marekani na mmoja wa watendaji na wawekezaji wa masuala ya sanaa na burudani nchini humo Tyrone Davis alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi.

Tyrone amemueleza Dkt. Abbasi kuwa wasanii wa muziki wa Tanzania wana vipaji, hivyo wanapaswa kutafutiwa namna ya kuingia zaidi katika soko kubwa kama la Hollywood kuanzia fursa za kurekodi na wasanii wakubwa, kusainiwa na rekodi kubwa na kukua zaidi hadi kushirikishwa katika matamasha makubwa.

“Kwa wale wa filamu ni muhimu nao washiriki filamu kubwa na sisi diaspora tulioko huku turudi katika nchi kama Tanzania na kuwekeza miundombinu ya kisasa ya sanaa kama studio, kupitia kampuni na mitandao yangu tutafungua njia hiyo kwa kuratibu pamoja programu ya kimkakati pamoja na Serikali ya Tanzania,” ameahidi Tyrone

Katika kipindi cha takribani miaka 20 katika kiwanda cha burudani nchini Marekani, Tyrone ameendelea kubaki mmoja wa watu wanaofahamiana na wadau muhimu wa Hollywood, akiwa amefanya kazi na wasanii nguli wa zamani akiwemo MC Hammer, Lionel Richie na produza mwenye tuzo 38 za Grammy, Quincy Jones.