Sojo kwanoga mradi wa EACOP

0
176

Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga unaendelea kushika kasi.

Kwa sasa wakandarasi kutoka kampuni nne tofauti wanashirikiana kujenga kiwanda kitakachotumika kuandaa mabomba na kuyaongezea uwezo wa kutunza joto pamona kupaka rangi.

Mratibu wa mradi huo wa EACOP, Asiad Mrutu amesema, kiwanda hicho kinajengwa katika kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora.

Akieleza hatua za ujenzi wa mradi huo akiwa katika eneo kinapojengwa kiwanda hicho Mrutu amesema, serikali inatoa ushirikiano wa karibu kwa wakandarasi hao katika kila hatua, ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

“Serikali inausimamia vema mradi huu ili kuhakikisha kila kitu kinapatikana kwa wakati ikiwepo vibali vya ujenzi kutoka taasisi mbalimbali za serikali na kurahisisha shughuli zote za mradi.” ameongeza Mrutu

Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki unatarajiwa kugharimu shilingi trilioni 11 hadi kukamilika kwake na kuzalisha ajira zaidi ya elfu kumi na fursa nyingine za kiuchumi kwa Taifa.