Sita mbaroni kwa kujeruhi waumini wenzao

0
166

Watu watatu wamejeruhiwa katika eneo la Maore chini kata ya Maore wilayani Same Mkoani Kilimanjaro baada ya kuvamiwa na waumini wenzao wakiwa katika sherehe ya maulid.

Kufuatia tukio hilo watuhumiwa Sita wamekamatwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na tukio hilo na vurugu zilizotokea katika eneo la madrasa ya Shamsia usiku wa Agosti 19, 2021.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja waliojeruhiwa kuwa ni Daud Bakari, Hamadi Juma na Rajab Ally huku akitaja chanzo cha vurugu hizo ni mgogoro wa uongozi wa msikiti ulioko katika kata hiyo.

Wakizngumza na TBC, baadhi ya majeruhi wa tukio hilo wamesema wakati wakiwa kwenye sherehe ya maulidi ghafla walivamiwa na kikundi cha waumini kutoka katika msikiti mwingine wakiwa na fimbo na virungi na kuanza kuwashambulia wakidai hawaruhusiwi kufanya maulidi katika eneo hilo, jambo ambalo liliwasababishia majeraha na wengine kupoteza fahamu.

Nae Sheikhe wa kata ya Maore, Mwinjuma Halfan ambaye pia ndiye kiongozi wa  madrasa ya Shamsia  iliyokuwa ikifanya maulid hayo ameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kusema kuwa limesababisha uharibifu katika madrasa yao.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.