Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Simba SC ina mengi ya kujifunza kwa Yanga SC kutokana na mafanikio iliyoyapata kwenye mashindano ya Afrika msimu huu ambapo ilifika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho.
Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma ambapo ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuleta hamasa kwa timu katika michezo ya Kimataifa kwa kununua kila goli linalofungwa.
Kwa hamasa hiyo Simba imepata shilingi Milioni 55 na Yanga shilingi Milioni 135, fedha ambazo ziliwasaidia katika maandalizi ya michezo yao.
Pia, ameipongeza Simba kwa kuendelea kufanya vizuri kimataifa na kufikia hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
“Kwa kipekee kabisa napenda kuipongeza timu ya Yanga kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika pamoja na kutoa Mfungaji Bora (Mayele) na Kipa Bora (Diara). Hakika timu ya Simba ina mengi ya kujifunza kutoka kwa timu ya Yanga,” amesema Dkt. Mwigulu.